Dkt. Mollel: Rais Samia ametoa fedha nyingi kupambana na magonjwa yasiyoambukiza

0
45

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka fedha nyingi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo eneo la manunuzi ya vifaa tiba kama vile CT-SCAN katika kila hospitali za Rufaa za mikoa pamoja kusaini mikakati kwa Wakuu wa Mikoa wote kuhusu masuala ya lishe kwenye kila mkoa.

Dkt. Mollel ameyasema hayo bungeni akijibu swali la Mbunge wa Viti Malumu, Bernabetha Mushashu aliyehoji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kutoa pesa za kutosha kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza nchini.

“Serikali imeweka fedha nyingi. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan hapa karibuni alisaini mikataba na Wakuu wa Mikoa kwenye eneo hili la lishe,” ameeleza Dkt. Mollel.

Aidha, amesema Serikali imeweka mikakati thabiti ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kuimarisha ushirikishwaji wa sekta mtambuka, kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma, kuwajengea uwezo watumishi ili kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti na kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Ameeleza mkakati mwingine wa mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ni kuunga mkono kwa Mpango wa Bima ya Afya kwa wote pindi utapoletwa bungeni ili kumpa haki kila mwananchi kupata matibabu bila malipo kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali ya Taifa.

Send this to a friend