Dkt. Mpango aagiza kasi ya usambazaji maji ili kutatua kero za maji

0
31

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Maji kuendelea na kasi ya usambazaji maji kutoka Ziwa Victoria ili kutatua adha ya ukosefu maji wanayopata wananchi kwa muda mrefu.

Ameyasema hayo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Bukene unaogharimu shilingi bilioni 29.3 katika hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Uduka Wilayani Nzega, ikwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tabora ambapo ameipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa inayofanya kuhakikisha maeneo yaliokabiliwa na changamoto ya maji yanafikiwa hususani kwa kutumia chanzo cha Ziwa Victoria.

Aidha, katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Tabora kuongeza juhudi katika kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuitaka Wakala wa Misitu Nchini (TFS) kuhakikisha miche inapatikana ili kuwezesha wananchi kupanda miti katika kipindi cha mvua kinapokaribia.

Vilevile, Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Bukene kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu.