Dkt. Mpango aagiza Magereza kuondoa matumizi ya ndoo kama choo kwa wafungwa

0
52

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Magereza kuchukua hatua zinazowezekana kwa kutumia rasiliamli zilizopo, kuondoa dhana ya kudhalilisha utu na kukiuka haki za binadamu kwa wafungwa.

Amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza unaofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Msalato mkoani Dodoma ambapo amesema ni muhimu kupunguza na hata kuondokana kabisa na matumizi ya ndoo magerezani kama choo.

Aidha Dkt. Mpango amelisisitiza Jeshi la Magereza kuzingatia na kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai pamoja na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuboresha huduma za urekebu na ufanisi wa Jeshi hilo.

Amesema taarifa hizo ziliainisha mambo mbalimbali yanayopelekea wafungwa wanaomaliza vifungo kufungwa tena kuwa ni pamoja na kukosekana kwa miongozo rasmi ya magereza ya namna ya kutekeleza programu za urekebu, kutokuwepo kwa programu za kutosha za huduma za kielimu na kisaikolojia kwa wafungwa na kukosekana kwa programu za kuwaandaa wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo.

Mbali na hayo, Dkt. Mpango amewasihi kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya juhudi kuwapatia wafungwa vifaa vitakavyowasaidia kujiendeleza kielimu wanapokuwa magerezani kama kompyuta, vitabu na vifaa vingine.

Send this to a friend