Dkt. Mpango aagiza ujenzi uwanja wa ndege Tabora ukamilike kwa wakati

0
49

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amezitaka Wizara ya Ujenzi pamoja na Wizara ya Uchukuzi kushirikiana kikamilifu ili mradi wa ujenzi na upanuzi wa Kiwanja cha ndege Tabora ukamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.

Ameyasema hayo leo mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanja cha ndege Tabora ambapo ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika mradi huo.

“Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi mnapaswa kutambua kuwa fedha hizi ni za wananchi hivyo zitumike vizuri kwa maendeleo ya wananchi kama ilivyokusudiwa,” amesema Dkt. Mpango.

Aidha, kuhusu usalama barabarani Dkt. Mpango ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani ili kuepuka ajali na kuwaonya wanaohujumu alama za barabarani kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 72 huku jengo la abiria likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja litakapokamilika.