Dkt. Mpango aagiza watendaji wanaokwamisha ujenzi wa barabara kuchukuliwa hatua
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Barabara ya Malagarasi – Uvinza (Kilometa 51.1) kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Machi 2025 kama ilivyopangwa.
Maelekezo hayo ni mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo akiwa ziarani mkoani Kigoma, ambapo amewasihi viongozi na watendaji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu pamoja na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaokwamisha ujenzi wa barabara hiyo.
Amewasihi watendaji wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Mkandarasi kutumia vema msimu huu wa kiangazi kuhakikisha wanafanya kazi kwa haraka bila kupoteza ubora unaotarajiwa ili barabara hiyo iweze kukamilika kabla ya ujio wa mvua.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupooza Umeme wa Msongo wa Kv 132 kilichopo Kijiji cha Nguruka Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma na kuipongeza Wizara ya Nishati kwa maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kimefikia asilimia 95.
Amesema serikali imedhamiria kuufungua Mkoa wa Kigoma ikiwemo upatikanaji wa umeme nafuu ili kuweza kuvutia zaidi wawekezaji.
Aidha, Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Nishati kufutilia mradi wa umeme wa Igamba uliyopo Wilaya ya Uvinza ili ukamilike kwa wakati na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha katika mkoa huo.