Dkt. Mpango ahimiza kupunguzwa gharama za kutumia huduma za kifedha

0
17

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa rai ya kupunguzwa kwa gharama za kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuongeza wigo wa dhamana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo pamoja na kutoa wito wa kuongezwa na kurahisishwa kwa miundombinu ya malipo ya pamoja ili kuchochea matumizi ya huduma rasmi za fedha.

Aidha, amewasihi wataalam na wadau wa huduma jumuishi za fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha hususani kwa vijana.

Amesema hayo leo wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es salaam.

Dkt. Mpango amewasihi watalaam hao kuhakikisha malengo yaliowekwa katika mpango huo wa tatu wa huduma jumuishi za fedha yanafikiwa kikamilifu ifikapo mwaka 2028 hususani kwa kuelekeza juhudi katika makundi ambayo hayajafikiwa ikiwemo watu wenye ulemavu, wakulima wadogo, wavuvi, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo.

Aidha, amesema huduma jumuishi za fedha ni miongoni mwa vipaumbele vya nchi pia ni lengo muhimu la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, hivyo huduma hiyo inayopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha watu wa makundi yote wanafikiwa.

Serikali yaagiza atakayeuza sukari kwa zaidi ya TZS 3,200 kwa kilo ashtakiwe

Halikadhalika, amesema ni vema kuendelea na jitihada za kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ili kuwajengea wateja imani ya kuendelea kutumia huduma hizo.

Send this to a friend