Dkt. Mpango: Amani na usalama ni nguzo muhimu kwa mifumo ya chakula

0
29

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla kutumia njia za usuluhishi wa amani katika kukabiliana na migogoro mbalimbali kwa kuwa amani na usalama ni nguzo muhimu kwa mifumo ya chakula.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula barani Afrika kwa Mwaka 2023 (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, amesema idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao sababu ya migogoro ambao ni pamoja na wakulima na wafugaji wamekatizwa maisha yao na uwezo wao wa kuzalisha chakula.

Aidha, amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapa wakulima wadogo pembejeo za bei nafuu, maarifa, ujuzi na mitaji ili kuongeza tija katika uzalishaji chakula pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuondoa ukandamizaji wa aina yeyote kwa wakulima ikiwemo kuhakikisha matumizi sahihi ya vipimo katika masoko ya mazao ya kilimo ili kuwalinda wakulima.

Mbali na hayo, Makamu wa Rais amesema mageuzi katika mifumo ya chakula yanaenda sambamba na ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo usafirishaji wa bidhaa za chakula, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuheshimu mipango ya biashara ya kikanda, hasa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA), kwa kuzingatia itifaki za kibiashara na kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha.

Send this to a friend