Dkt. Mpango aziagiza Halmashauri kuwasaidia vijana kiuchumi

0
40

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa vijana nchini kujiepusha na matendo yote yasioendana na maadili ya taifa ili waweze kuaminika katika taasisi za kifedha, katika uongozi pamoja na kuwa raia wema.

Amesema hayo leo wakati akifungua Kongamano la Vijana la Mkoa wa Dodoma ambapo ameagiza kongamano hilo kujadili kwa kina nafasi na wajibu wa wazazi, walezi, viongozi wa dini, kimila, vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na vijana wenyewe katika kujenga na kutunza maadili ya vijana wa Kitanzania.

Aidha, ameziagiza Halmashauri zote nchini kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi kwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uzalishaji mali kwa vijana ikiwemo kuanzisha kongani zinazoendana na fursa zilizopo kwenye maeneo, kuwaunganisha vijana na fursa za mitaji, kuhamasisha na kusimamia urasimishaji wa vikundi vya vijana ili viweze kutambulika.

Mkandarasi aagizwa kulipa bilioni 2 kwa kutokamilisha mradi kwa wakati

Maagizo mengine ni pamoja na kutengeneza kanzidata ya vijana na ujuzi au taaluma zao ili kuweza kuwaunganisha na fursa mbalimbali zinazojitokeza, kuhamasisha na kuwezesha vijana kuunda klabu za mazingira na kuunganisha vijana katika uzalishaji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kitaasisi zitakazosaidia kutoa ufumbuzi wa changamoto zao.

Ameongeza kuwa Serikali ina dhamira ya kuona vijana wanaendelezwa na wanawezeshwa kushiriki katika ujenzi wa Taifa, ambapo imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, urasimishaji na kuendeleza biashara kwa vijana 2,497 pamoja na kukamilisha kazi ya kuboresha mwongozo wa utoaji mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo kwa sasa unatoa mikopo kwa vijana walio katika vikundi, mtu mmoja mmoja na kampuni.

Send this to a friend