Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kukabiliana na upungufu wa fedha za maendeleo ili kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) duniani.
Amesema hayo wakati akichangia katika mjadala wa viongozi wa ngazi ya juu kuhusu ufadhili wa maendeleo uliokuwa na dhima ya kutafuta suluhisho la kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Makamu wa Rais amesema ili kushawishi sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ni vema mataifa yakajielekeza katika kuweka sera rafiki kwa sekta binafsi kwani ni miongoni mwa wadau muhimu katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.
Halikadhalika amesema kwa kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa, Tanzania imefanikiwa kuwa na njia mbalimbali za ufadhili ambazo ni rafiki kwa sekta binafsi ikiwemo kutengeneza ramani ya wawekezaji ya malengo ya maendeleo endelevu.
Ameongeza kwamba katika uboreshaji wa miundombinu, Tanzania imetumia mbinu ya Ufadhili wa Mikataba ya Ujenzi na Ununuzi wa Kihandisi (EPC+F) ili kuongeza ufadhili wa sekta binafsi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri.