Dkt. Mpango: Tanzania tumefanikiwa kwenye malengo ya mendeleo endelevu 

0
31

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania itaendelea kuchangia katika juhudi za kuleta na kudumisha amani barani Afrika na kwingineko duniani na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono katika mipango ya kikanda ya kuleta amani katika maeneo yenye vita barani Afrika.

Akiihutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani, amesema hadi kufikia Machi 2023 Tanzania imekuwa ndio mchangiaji mkubwa wa 12 kati ya nchi 125 katika shughuli za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.

Dkt. Mpango ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuwakemea kwa uwazi wale wote wanaoshiriki katika kuchochea migogoro barani Afrika kwa lengo la kuuza silaha au kupata utajiri wa rasilimali zilizopo na kwamba dunia inahitaji kuwekeza zaidi katika mazungumzo na diplomasia katika kutatua migogoro ya kivita ili kuifanya kuwa sehemu salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, amesema Tanzania imedhamiria kutekeleza kikamilifu malengo ya maendeleo endelevu kama inavyotarajiwa, ambapo Julai mwaka huu iliwasilisha Ripoti ya pili ya Hiari ya Taifa (VNR) ambayo inaonyesha kwa ujumla kumekuwa na mafanikio makubwa kwa lengo namba 2 – 7 kwa ongezeko la uwiano wa kutosha wa chakula, upatikanaji wa dawa muhimu, kupungua vifo vya chini ya miaka 5, hatua muhimu katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, uboreshaji wa upatikanaji wa maji mijini na vijijini pamoja na utoaji wa huduma ya nishati ya umeme.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu umekuwa wa kukatisha tamaa hasa kutokana na kutotekelezwa kwa ahadi za kifedha na teknolojia kutoka kwa nchi zilizoendelea duniani na upungufu wa fedha katika nchi nyingi za Afrika.

Send this to a friend