Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Uchukuzi nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ili kuleta ushindani katika biashara.
Ameyasema hayo leo katika hafla ya mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-MAX 9 iliyokuwa ikitokea Seattle, Marekani na kupokelewa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
“Kuwasili kwa ndege hii ya kisasa ambayo inafanya idadi ya ndege katika shirika letu kufikia 14 ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuiwezesha ATCL kutoa huduma bora na ya ushindani, huku ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max 9 na Boeing 787-8 Dreamliner, zikitarajiwa kuwasili nchini kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2023 na mwezi Machi 2024,” amesema.
Aidha, amesema ili kuongeza ufanisi wa Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT) katika kutoa mafunzo ya urubani, mwezi Juni, 2023, Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege moja mpya ya mafunzo yenye injini mbili aina ya Beechcraft Baron G58 toka Kampuni ya Textron Aviation Inc. ya Marekani ambayo inatarajiwa kuwasili katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Hivyo, naelekeza Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kuhakikisha kuwa ndege hizo zinazonunuliwa kwa fedha nyingi za umma zinatunzwa kwa kuzingatia masuala ya usalama ili ziweze kutumika kutoa mafunzo kwa muda mrefu zaidi,” ameeleza.
Mbali na hayo, Dkt. Mpango ameitaka kampuni ya ATCL kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanatoa huduma bora huku akibainisha kuwa serikali haitovumilia uzembe wowote ambao ulifanyika katika kipindi cha nyuma.