Dkt. Mpango: Vijana changamkieni fursa zinazotolewa na Rais Samia

0
14

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kujipatia kipato pamoja na kukuza pato la nchi.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nanenane leo Agosti 01, 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

“Kwa dhati kabisa namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa uamuzi wake wa kutoa msukumo katika uwezeshaji wa vijana kupata ajira kupitia miradi ya jenga kesho iliyo bora (Building a Better Tomorrow – BBT), kwa upande wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Hivyo, nawasihi vijana kuchangamkia fursa hizi ili kujipatia ajira na kukuza uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla,” amesema.

Aidha, amesema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kukuza kipato na kutoa ajira kwa wananchi.

“Kwa sababu hiyo, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka TZS bilioni 275 mwaka 2021/2022 hadi TZS 295 bilioni mwaka 2023/24 na ile ya Wizara ya Kilimo kutoka TZS bilioni 294.16 kwa mwaka 2021/2022 hadi TZS bilioni 970.78 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 330.02,” ameeleza.

Katika hotuba yake Dkt. Mpango amebainisha kuwa thamani ya mauzo ya mahindi nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 57.09 [TZS bilioni 140.2] kwa mwaka 2021 hadi Dola milioni 71.54 [TZS bilioni 175.6] mwaka 2022 na thamani ya mauzo ya ufuta kutoka Dola za Marekani milioni 123 [TZS bilioni 301.96] mwaka 2021 hadi Dola milioni 143.78 [TZS bilioni 352.97] mwaka 2022.