Dkt. Mpango: Wazalishaji zingatieni kanuni za ushindani za masoko

0
13

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amefunga Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba yaliofanyika jijini Dar es salaam kuanzia Juni 28, 2022.

Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amewaasa wazalishaji hapa nchini kuzingatia kanuni za ushindani katika soko, ikiwemo kuheshimu mikataba na kuzalisha bidhaa bora na za viwango vya juu, pamoja na kuzalisha bidhaa zenye mahitaji makubwa nchini kama vile chakula na bidhaa za ujenzi.

Ameongeza kuwa, Watanzania hawana budi kujipanga ili kutumia kikamilifu eneo huru la kibiashara la Afrika (AfCTA) lenye takribani watu bilioni 1.3 katika kuuza bidhaa na kuongeza wigo wa soko la bidhaa za Tanzania.

Awali akitembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo, amewasihi watoaji huduma za kifedha zikiwemo benki kuendelea kupunguza riba ili kuwapa fursa wajasiriamali wadogo kupata mitaji na kufanya biashara.

Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema wizara itahakikisha Tanzania inaenda katika eneo huru la kibiashara la Afrika kama washindani na sio washiriki.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema katika maonesho hayo kumekuwa na ongezeko la ushiriki kutoka kampuni 3,200 kwa mwaka 2021 mpaka 3,425 kwa mwaka 2022.