Dkt Mpango: Zimamoto wanachelewa kufika kwa sababu ya ujenzi holela

0
50

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakati ili tija na ufanisi viweze kuonekana kwa wananchi.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kituo kikuu cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam kilichogharimu shilingi bilioni 4.09 amesema katika kuadhimisha miaka 59 ya Muungano ni vema jeshi hilo kujipima ni kwa kiasi gani limefanikiwa katika utoaji huduma ya zimamoto na uokoaji nchini.

Amesema baadhi ya changamoto ya uchelewaji kufika eneo la tukio ni ujenzi holela pamoja na vituo vya jeshi hilo kuwa mbali na makazi ya wananchi, hivyo ameiasa Wizara ya Ardhi na mamlaka zinazohusika kuendelea kudhibiti ujenzi holela ili kuhakikisha maeneo ya makazi yanakuwa na barabara za kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wakati wa dharura.

Aidha, ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga zaidi vituo vya zimamoto na uokoaji, akiongeza kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo katika Wilaya zote nchini ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati na kuzuia athari zaidi.

Halikadhalika Dkt. Mpango ametoa rai kwa jeshi hilo kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa na ukaguzi husika unafanyika kabla ya ujenzi wa vituo vya mafuta vinavyojengwa karibu na makazi ya watu ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.

Send this to a friend