Dkt. Mwigulu aishukuru China ufadhili wa ujenzi wa SGR Mwanza – Isaka

0
53

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ameishukuru China kwa kufikia hatua za mwisho za kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaendelea hivi sasa kwa kipande cha tano kuanzia Mwanza hadi Isaka na kuahidi kufanyia kazi maombi mengine ya kipande cha sita kinachoanzia Tabora hadi Kigoma.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili masuala muhimu ya ushirikiano kati ya China na Tanzania uliodumu kwa miaka 60 sasa.

Dkt. Nchemba amesema Mradi wa Reli ya Kisasa ni muhimu kwa uchumi na maendeleo ya Watanzania na kwamba ujumbe wa Balozi Chen kwamba China kupitia taasisi zake inakamilisha taratibu za ndani za kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo umepokelewa kwa mikono miwili na Serikali.

Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian, amesema nchi yake inauchukulia uhusiano wake na Tanzania kuwa ni wa kipekee na kwamba maelekezo ya Kiongozi wa nchi hiyo, XI Jinping ni kwamba anataka uhusiano huo uwe wa mfano na kielelezo barani Afrika.

Alisisitiza kuwa maombi ya Tanzania ya kupata fedha kwa ajili ya kipande cha tano na mengine ya kutaka ufadhili wa ujenzi wa kipande cha sita yamepokelewa na kwamba uamuzi wake utatolewa hivi karibu baada ya mambo machache yanayofanyiwakazi kukamilika.

Aidha, alieleza kuwa mpango wa miaka mitatu wa China wa ushirikiano kati yake na nchi za Afrika (FOCAC), umeitengea Tanzania kiasi kikubwa cha fedha ambazo zitaelekezwa katika miradi inayogusa masuala ya uchumi wa kijani, biashara na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Send this to a friend