Dkt. Mwigulu akanusha taarifa ya Tanzania kufilisika

0
91

SWaziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amekanusha taarifa inayosambaa mitandaoni ikieleza kwamba serikali imefilisika kiasi cha kushindwa kulipa madeni kadhaa yalliyosababisha kusuasua kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere na migogoro katika kampuni ya Yapi Merkezi inayohusika na ujenzi wa mradi wa reli ya Kisasa (SGR).

Dkt. Mwigulu amekanusha taarifa hiyo leo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii akiwataka Watanzania kupuuza taarifa iliyochapishwa na ukurasa wa Tanzanialeaks katika mtandao wa X (zamani Twitter) Julai 18, 2024 ambayo ilieleza kuwa imepata taarifa hizo kutoka Wizara ya Fedha.

Taarifa hiyo pia iliambatana na picha iliyonaswa katika kioo cha simu yenye ujumbe kutoka kwa mtu anayedaiwa kutoka wizarani ukieleza kuwa serikali imefilisika na miradi mingi kukwama kutokana na makandarasi kutolipwa fedha zao kwa wakati hivyo kupelekea baadhi ya wafanyakazi kuachishwa kazi kwenye miradi hiyo.

Katika kutolea ufafanuzi wa jambo, hilo Dkt. Mwigulu ameeleza kwamba taarifa hiyo haina ukweli wowote na ni ya watu na imetolewa na watu wenye nia ovu kuitakia mabaya serikali.

“Serikali haijafilisika, ameandika hatujalipa bwawa – uongo mtupu, Bwawa la Mwl. Nyerere hatudaiwi hata Invoice moja na wiki jana tumewasha na mtambo wa 7, (Sasa tumeshawasha 7, 8 & 9 kila mmoja 235MW),” amesema.

Aidha kuhusu madai ya kampuni ya Yapi Merkezi, Dkt. Mwigulu ameeleza kuwa kampuni hiyo ilikuwa na matatizo madogo ambayo yanaendelea kutatuliwa ikiwamo malipo kulipwa.

“Malipo yameendelea kulipwa kwenye sekta zote na mengine yapo kwenye hatua za mwisho za malipo. Waongo buana amesahau kwamba ndio tuko wiki ya pili ya mwaka mpya wa fedha,” ameeleza Dkt. Mwigulu.

Send this to a friend