
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuongeza rasilimali watu, bajeti, miundombinu na kufanya marekebisho ya kisheria ili kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Cate Convention Centre, mkoani Morogoro, Dkt. Mwigulu amesema kwa juhudi hizo, TAKUKURU imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 60.2, ambazo zimeelekezwa katika huduma muhimu za jamii zikiwemo afya, elimu, maji, umeme na miundombinu.
“Rushwa inadhalilisha utu wa binadamu na inazorotesha utoaji wa huduma za jamii. Ni lazima tuchukue hatua za kuzuia kabla haijazalisha madhara. Rushwa ni ajenda ya kitaifa inayohusu pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesisitiza Dkt. Nchemba.
Ameongeza kuwa taasisi za Serikali lazima zibainishe na kuziba mianya ya rushwa hususan katika maeneo ya manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi, na usimamizi wa mikataba, kwani zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya Serikali hupitia katika maeneo hayo.
Waziri Mkuu pia amewahimiza Watanzania kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, akisisitiza usiri wa watoa taarifa. Aidha, amewahimiza kushirikisha sekta binafsi, wadau wa kimataifa, pamoja na vijana na wanawake katika jitihada za kupambana na rushwa.







