Dkt. Mwigulu: Fedha zisizotumika hadi mwisho wa mwaka hurudi Mfuko Mkuu wa Serikali

0
20

Serikali imesema kuwa fedha ambazo hazijatumika hadi mwisho wa mwaka hurudi Mfuko Mkuu wa Serikali ikiwa ni utaratibu wa kusimamia uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha zilizotengwa katika bajeti.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmad Katani, aliyetaka kujua lini Serikali itarejesha fedha za miradi zilizochukuliwa na Hazina.

Dkt. Nchemba, amefafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Bajeti SURA 439, fedha ambazo hazijatumika hadi mwisho wa mwaka zinakoma matumizi yake na kurudishwa Mfuko Mkuu wa Serikali.

Ameongeza kuwa iwapo kuna miradi au shughuli ambazo hazijakamilika, fungu husika linatakiwa kutenga bajeti na kuwasilisha maombi kwa kuambatisha hati za madai au nyaraka za utekelezaji wa miradi hiyo.

Dkt. Nchemba amesema kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa miradi yote inatekelezwa ili kuleta maendeleo kwa wananchi.