Dkt. Mwinyi aihakikishia Uingereza kuendelea kudhibiti ugonjwa wa Trakoma

0
3

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameihakikishia Uingereza kwamba Zanzibar inaendelea na mikakati na juhudi kubwa ya kuhakikisha inadhibiti na kuumaliza ugonjwa wa Trakoma (Trachoma) nchini.

Ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Princess Sophie (Duchess of Edinburgh) aliyepo Zanzibar kwa ziara ya siku sita kutembelea miradi mbalimbali ya Afya inayotekelezwa na taasisi tofauti ambazo yeye ni mlezi wake.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema hatua iliyofikiwa na Zanzibar ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali inatokana na juhudi kubwa na misaada ya afya inayotolewa na Uingereza, na kumuahidi kuwa Zanzibar itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kupambana na magonjwa, hasa yasiyoambukiza (NCDs), yanayoathiri ustawi wa jamii.

Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi amemuhakikishia Princess Sophie kuwa Zanzibar inaendelea kuweka mkazo zaidi na kuhakikisha huduma bora za sekta ya afya, hususan kuimarisha huduma za kitengo cha uzazi salama cha mama na mtoto, na kuwataka wafadhili pamoja na washirika wengine wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Kwa upande mwingine, Princess Sophie ameipongeza Zanzibar kwa hatua iliyofikia ya kudhibiti ugonjwa wa Trakoma kwa kiasi kikubwa na kufikia mapema malengo yaliyowekwa na Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ya kumaliza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Princess Sophie (Duchess of Edinburgh) ni mke wa mtoto wa mwisho wa aliyekuwa Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, Prince Edward, ambaye ni mdogo wa Mfalme wa sasa wa Uingereza, Charles III.