
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amewasisitiza mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kuzingatia diplomasia ya uchumi na kuzitangaza fursa za uwekezaji ziliopo.
Ameyasema hayo alipozungumza na mabalozi wa Tanzania wa nchi za Rwanda, Zimbabwe, Sweden na Msumbiji waliofika Ikulu kumuaga kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi baada ya kuteuliwa hivi karibuni.
Amewahimiza mabalozi hao kufanya juhudi maalum za kuitangaza Sera ya Uchumi wa Buluu na Utalii katika mataifa hayo ili kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza nchini.
Amesema Zanzibar bado inahitaji wawekezaji wengi hususan katika sekta hizo Kuu za kipaumbele kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi ikiwemo Uvuvi, Utalii na Mafuta na Gesi.
Kadhalika, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa suala la mahusiano ya Kimataifa hivi sasa limeelekezwa zaidi katika uchumi hivyo wanapaswa kuzingatia zaidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.