
Waziri Mkuu Mteule wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hatowavumilia watumishi wa umma wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania.
Ameyasema hayo leo Novemba 13, 2025 baada ya kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania ambapo ameahidi kufanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu na jitihada kubwa ili kuweza kukidhi matarajio ya Watanzania.
“Watumishi wa Umma na Watanzania wote tuwe tayari. Lazima twende kwa gia ya kupandia mlima, lazima twende kwa gia ya kupita kwenye bahari yenye mawimbi, lazima twende kwa gia ya kupita kwenye anga lenye mawingu. Lazima chombo kifike salama na watu wake wakiwa salama,” ameeleza.
Aidha, Dkt. Nchemba amesema yale yote yaliyoongelewa kwenye Dira, kwenye Ilani ya Uchaguzi, ahadi za Rais Samia Suluhu, ahadi za wabunge, na yale ambayo Watanzania wanatamani yatimie, yatatimia endapo taifa litaendelea kumtanguliza Mungu na endapo taifa litakuwa na amani.
“Tumtangulize Mungu hata kwa yale tunayoona ni magumu ili tuweze kuhakikisha kwamba Mungu anatusaidia kupata ufumbuzi wake kwa sababu kwake yote ni mepesi,” amesema.
Mbali na hayo, amesisitiza kuwa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lazima yatekelezwe na kwamba atasimamia kwa uadilifu yale yote yaliyo dira ya Rais Samia Suluhu katika kutatua kero za Watanzania.







