
Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajiwa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la uzinduzi wa ukarabati wa reli ya TAZARA, Novemba 20, 2025 Jijini Lusaka, nchini Zambia.
Dkt. Nchimbi amewasili nchini humo leo na kupokelewa na Waziri wa Afya wa Zambia, Dkt. Elijah Muchima, Balozi wa Tanzania nchini Zambia Balozi, Luteni Jenerali Mathew Mkingule, maafisa waandamizi wa Zambia na Tanzania pamoja na vikundi mbalimbali vya ngoma vilivyoandaliwa kwa heshima yake.
Pamoja na viongozi wengine, Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Machibya Masanja pamoja Mkurugenzi Mkuu TASAC, Mohamed Salum.








