
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi, viongozi wa chama hicho pamoja na viongozi wa serikali kwa ushirikiano na imani waliyomuonesha kwa kipindi chote cha uongozi wake.
Mbele ya maelfu ya wananchi wa Mtwara Mjini leo Ijumaa Septemba 26, 2025 kwenye Viwanja vya Sabasaba, Dkt. Samia ameomba kuaminiwa tena ili kuendeleza maendeleo na ustawi wa Tanzania.
“Mafanikio katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hatuwezi kusema ni jitihada za mtu mmoja ila nawashukuru sana Viongozi wa Chama na serikali katika Mikoa yote ya Tanzania kwa imani na ushirikiano uliotuwezesha kutekeleza mipango mingi ya maendeleo katika miaka mitano iliyopita na huu ushirikiano kutoka kwa Viongozi wa nchi nzima kuanzia Ngazi za Vitongoji.” Ameeleza Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameeleza kujipanga kuendelea kuustawisha Mkoa huo kwa miradi ya maendeleo pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya usafiri na usafirishaji, akitangaza ujenzi wa reli mpya ya kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay ili kurahisisha biashara kati ya Mtwara na nchi za Msumbiji na Malawi.
Dkt. Samia amehitimisha ziara yake ya Kampeni mkoani Mtwara tayari kwa kuendelea na mikutano yake ya kampeni kwenye mikoa mingine ya Tanzania.






