
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu amesema ikiwa wananchi watampa ridhaa Oktoba 29, 2025 kazi itakayoendelea kuupa hadhi utu wa Mtanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata mahitaji muhimu.
Ameyaeleza hayo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Nakapanya mkoani Ruvuma waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa kampeni, akiahidi kujenga kituo cha Afya Kata ya Namiungo mkoani Ruvuma pamoja na ukamilishaji wa Zahanati kwenye eneo hilo.
“Kazi inayoendelea ni kwenda kuheshimu na kuupa hadhi utu wa mtu ndio maana tunasema kazi na utu, tunasonga mbele,” amesema Dkt. Samia.
Katika hatua nyingine, amesema anaifahamu changamoto ya maji kwenye eneo hilo, akiahidi kuwa Ilani ya CCM imeagiza kila mwananchi apate maji safi na salama, hivyo suala hilo atalisimamia kikamilifu kama sehemu ya dhamira yake ya kulinda na kutunza utu wa Mtanzania.








