
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu amesema kufanikiwa kwa miradi mingi ya maendeleo nchini kumetokana na usimamizi mzuri wa fedha na kumudu upunguzaji wa viwango vya rushwa nchini.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni Mjini Nzega Mkoani Tabora, amewapongeza watumishi wa umma na wa sekta binafsi nchini kwa kuendelea kujiepusha na vitendo vya rushwa na udhibiti wa mianya yake.
Rais Samia amesema nchi ambazo zimekuwa zikitawaliwa na rushwa ni nadra kuzungumzia mafanikio kwenye sekta za kijamii kama ambavyo kampeni za CCM zimekuwa zikizungumza kuhusu mafanikio ya sekta ya maji, afya, miundombinu elimu na nyinginezo.
“Kwa pamoja tuwapongeze watumishi wa serikali, mashirika na Watumishi wa sekta binafsi wanafanya kazi nzuri na wamesimama vyema katika kupunguza viwango vya rushwa kama takwimu mbalimbali za Kimataifa zinavyoeleza na ndio maana maendeleo yanaonekana nchini, nchi zilizotawaliwa na rushwa hawayazungumzi tunayoyazungumza sisi hapa kwahiyo ndugu zangu watanzania tujipongeze sana,” amesema.
Aidha, amesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo wa dhahabu eneo la Lusu Mkoani Tabora, akisema tayari serikali ya awamu ya sita ilitoa leseni 77 kwa wachimbaji wadogo wa Nzega, akiwashukuru pia wachimbaji wadogo nchini kwa mchango wao wa zaidi ya asilimia 40 kwenye pato la Taifa.








