
Rais Samia Suluhu amesema hakutakuwa na vurugu yoyote siku ya kupiga kura kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kulinda amani.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Gombani ya Kale, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar, amesema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu, Watanzania wasiingie kwenye migogoro dhidi ya watu wenye nia ovu, badala yake wawapuuze kama ambavyo amekuwa akifanya.
“Nataka niwaambie kwamba katika kipindi cha miaka hii mitano iliyopita tumejitahidi sana kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na amani ndani ya nchi yetu, hamjasikia lolote na mkisikia labda ni ajali watu wamekufa na labda mtu ambaye mwenyewe atakwenda kuchokoza mwenyewe na kuvunja amani ndiye atakayeshughulikiwa.
Hata wale waliovuka mipaka na kutaka kuleta vurugu ndani ya nchi yetu tuliwashughulikia na hawajathubutu kurudi tena. Niwaombe sana ndugu zangu katika kipindi hiki ni kipindi wengine wanatumia kuchokozana,” amesema.
Ameongeza kuwa “Tusiende kuvunja amani kwa sababu ya uchaguzi, sisi wote ni wamoja, kwahiyo sitafurahi kuona ndugu huku Makunduchi au Pemba kapigwa kaumizwa. Sisi wote niombe sana tutunze amani na utulivu na niwatoe hofu kwamba tarehe za kupiga kura hakutakuwa na vurugu yoyote, tokeni kwa wingi kapigeni kura, Vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kuilinda nchi hii na mimi ndiye Amiri Jeshi Mkuu ninayesema hapa.”







