Dkt. Samia: Vipaumbele vyetu ni kuhakikisha wanawake wanazifikia njia za kuwainua kiuchumi

0
42

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) unaweza kutoa fursa za kuwainua watu milioni 30 wa Afrika kutoka umaskini uliokithiri na kuongeza kipato cha Waafrika milioni 60 ambao wengi wao ni wanawake na vijana.

Ameyasema hayo leo wakati aliposhiriki Mkutano wa Mtandao wa Viongozi Wanawake wa Afrika uliofanyika Zanzibar ambapo amesema vipaumbele vilivyopo ni kuhakikisha wanawake wanazifikia njia za kuwainua kiuchumi ikiwemo kupata mikopo, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwasaidia kupata ardhi.

“Tunataka kuhakikisha kwamba wanawake wanaingia kwenye masoko ya kikanda na kuyatumia masoko hayo kama hatua ya kwenda mbali zaidi hadi kwenye masoko ya nje,” amesema Dkt. Samia.

Chama tawala Namibia chamchagua mgombea Urais mwanamke

Aidha, amefafanua kuwa katika kuongeza nafasi za wanawake katika uongozi, idadi ya wanawake imeongezeka kutoka mwaka 2005 hadi kufikia mwaka 2022 ambapo katika nafasi za wakuu wa mikoa wanawake wameongezeka kutoka asilimia  10 hadi asilimia 23, huku wakuu wa Wilaya wakiongezeka kutoka asilimia 19 hadi asilimia 25 mwaka huu.

Rais Dkt. Samia ameendelea kutaja nafasi hizo ambapo katika nafasi za ubalozi, amesema mabalozi wa kike wameongezeka kutoka asilimia 3 mwaka 2005 hadi asilimia 21 mwaka 2022.

Naye Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde amesema ni lazima wanawake wawezeshwe kushika nafasi katika maeneo mbalimbali ya uongozi ili kuimarisha usawa pamoja na kuondoa vizuizi ambavyo vinawarudhisha nyuma wanawake.

Send this to a friend