Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Balozi Dkt. Wilbrod Slaa amekiri kuudhika na maneno yaliyotolewa na baadhi ya wananchi yanayoeleza kuwa ‘Mbowe sio gaidi.’
Dkt. Slaa ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden amesema hayo huku akiwataka wananchi kuacha suala hilo mikononi mwa mahakama ambayo ndio chombo cha haki.
“Niliudhika tangu siku ya kwanza na maneno ‘Mbowe si gaidi.’ Mimi ni nani kusema Mbowe si gaidi? amehoji mwanasiasa huyo huku akisema hakuna sehemu duniani wananchi husema fulani si mhalifu.
Ameongeza kwamba hana chuki na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na kwamba mara kadhaa wamekutana, wakabadilishana namba za simu, lakini hakuna aliyempigia mwenzake.
Ameongeza kwamba kuna sura inayojitokeza kwa kugeuza kwenda mahakamani kwenye kesi hiyo kama sehemu ya siasa, jambo ambalo binafsi hakubaliani nalo.
“Sikwenda kwa sababu sikubaliani na principe [kanuni] inayotumika ya kwenda kule. Halafu mnatoka pale mnaanza kwenda kujipiga picha na mko kwenye mitandao. Hii ni siasa, mimi sichezi siasa. Mimi nikienda kumtembelea Mbowe, nitamtembelea Mbowe. Najua nyumbani kwake, nitaenda hata kwa watoto wake niwaambie jamani poleni,” amesema Dkt. Slaa akijibu swali kwanini hajaonekana mahakamani.
Ameongeza kwamba yeye atamuombea Mbowe ili Mungu atende haki, kwa sababu haki ndio kitu kinachotakiwa.
Dkt. Slaa alijiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu na uanachama wa CHADEMA mwaka 2015 baada ya ujio wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambaye alipewa nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka huo.
Novemba 2017 aliteuliwa kuwa Balozi, na Februari 2018 alipangiwa kituo kwenda Sweden, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 2021.