Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Wilbrod Slaa amethibitisha kushiriki katika maandamano ya CHADEMA yanayotarajiwa kufanyika mkoani Mwanza Februari 15, mwaka huu.
Hayo yameelezwa na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Zacharia Obad wakati wa ukaguzi wa uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani humo, ambapo maandamano hayo yanatarajiwa kuhitimishwa.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Dkt. Slaa ameithibitishia jamii kwamba atashiriki katika maandamano hayo, akisema kuwa, “Ni kweli nitashiriki na nitakuwepo.”
CHADEMA waruhusiwa kuandamana Mwanza, waonywa kutoikejeli Serikali
Mbali na Dkt. Slaa, wengine waliothibitisha kushiriki ni pamoja na wakili Boniface Mwabukusi, Mdude Nyagali (mwanaharakati), pamoja na viongozi wa juu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.
CHADEMA ilitangaza kuwa lengo la maandamano hayo ambayo yalianzia mkoani Dar es Salaam Januari 24, mwaka huu ni kuishinikiza serikali kuweka mpango wa kupunguza ugumu wa maisha, kufanya marekebisho ya kikatiba yenye kuwezesha uchaguzi huru na haki na kuendeleza mchakato wa katiba mpya.