Dkt. Tulia aipongeza CRDB kupunguza riba mikopo ya wanawake kutoka 24% hadi 14%

0
22
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba kwa mikopo ya wanawake wajasiriamali inayopatikana kupitia huduma ya “CRDB Malkia” hadi kufikia asilimia 14 kwa mwaka.


Akitoa hotuba yake katika hafla ya uzinduzi wa “CRDB Malkia” iliyokuwa na kauli mbiu ya “Fanikisha Zaidi na CRDB Malkia”, Dkt. Tulia alisema hatua ya Benki ya CRDB kupunguza riba kwa asilimia 10 kutoka asilimia 24 iliyokuwa ikitozwa mwanzo itasaidia wanawake wengi zaidi kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo.


“Kupungua kwa riba ina maana inapunguza mzigo mkubwa wa marejesho kwa wanawake na kuwafanya kuwa na fedha nyingi kwa ajili ya uwekezaji katika biashara zao na hivyo kupelekea kufanikisha zaidi,” alisema Dkt. Tulia. Dkt. Tulia alisema pamoja na tafiti kuonyesha wanawake wamekuwa na ushiriki mkubwa katika shughuli za uchumi nchini, kwa asilimia 54, ni asilimia 60% tu ya wanawake ndio wenye kufikiwa na huduma rasmi za kifedha.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Acksonakihutubia katika uzinduzi wa huduma ya CRDB Malkia ya Benki ya CRDB inayolenga katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini. Katika uzinduzi huo Benki ya CRDB imetangaza kupunguza riba ya mikopo kwa wajasiriamali kutoka asilimia 24 hadi asilimia 14, iliyofanyika leo katika hoteli ya Hyatt, jijini Dar es salaam. Picha zote na Othman Michuzi.

“Niwapongeze pia kwa kuboresha masharti ya dhamana ili kutoa fursa kwa wanawake wengi zaidi kuweza mikopo,” aliongezea Dkt. Tulia huku akiwataka wanawake pia wajitokeze kwa wingi kufungua akaunti ya Malkia itakayosaidia kufanikisha malengo yao kwa kujiwekea akiba kidogokidogo jambo litakalosaidia kujenga imani kwa taasisi za fedha.


“Mimi ni mmoja wa wanawake waliofungua akaunti ya Malkia wakati ikianzishwa mwaka 2009, nimefurahi kuona leo hii Benki yetu ya CRDB ikifanya maboresho yatakayoweza kumkomboa mwanamke,” aliongezea Dkt. Tulia.

Dkt. Tulia alisema jitihada hizi zinazofanywa na Benki ya CRDB katika uwezeshaji wa makundi mbalimbali ya wananchi zimekuwa na msaada mkubwa katika kuisaidia Tanzania kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi wa kati.


“Nimefurahi kuona leo hii tukiwa tunajivunia kuwa nchi ya uchumi wa kati, Benki yetu ya CRDB inaendelea kutubeba wanawake na kuwezesha kufikia malengo yetu ya nchi na dunia katika kuwa na usawa katika ushiriki katika shughuli za Maendeleo kama ilivyoainishwa katika mpango wa Maendeleo Endelevu 2030 wa umoja wa mataifa,” alisema Dkt. Tulia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akihutubia katika uzinduzi wa huduma ya CRDB Malkia ya Benki ya CRDB inayolenga katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini. Katika uzinduzi huo Benki ya CRDB imetangaza kupunguza riba ya mikopo kwa wajasiriamali kutoka asilimia 24 hadi asilimia 14.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema huduma ya CRDB Malkia imelenga katika kumtambua, kumpa nafasi na kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kufikia malengo yake kupitia mikopo ya biashara na ujasiriamali, kujiwekea akiba kwa akaunti ya Malkia na mafunzo ya uendeshaji biashara.


“Mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Benki yetu tayari ilikuwa imekwisha toa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 600 kwa wanawake zaidi ya elfu 55,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa zaidi ya wanawake 30,000 tayari wameshajiunga na akaunti ya Malkia.


Nsekela alisema pamoja na mafanikio ambayo Benki ya CRDB imeyapata katika kumuwezesha mwanamke, bado idadi ndogo ya wanawake wamekuwa wakijitokeza kupata huduma kutokana na changamoto ya riba, masharti magumu ya dhamana na kukosa uelewa wa huduma za kifedha. “Tukiwa Benki ya kizalendo inayothamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa letu, tukasema ni vyema tukatafuta suluhisho la changamoto hizi ili kuweza kumsaidia mwanamke kufankisha malengo yake zaidi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akifafanua jambo katika uzinduzi wa huduma ya CRDB Malkia ya Benki ya CRDB inayolenga katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini. Katika uzinduzi huo Benki ya CRDB imetangaza kupunguza riba ya mikopo kwa wajasiriamali kutoka asilimia 24 hadi asilimia 14.

Nsekela alisema wanawake sasa hivi wataweza kupata mikopo kwa riba ndogo ya asilimia 14 kulinganisha na asilimia 24 iliyokuwa ikitozwa mwanzo huku masharti ya upatikanaji wa mikopo yakirahisishwa kwa kiasi kikubwa.

“Kupungua kwa riba kuna maana wanawake sasa wanaweza kukopa zaidi na kwa gharama nafuu kulinganisha na mwanzo hivyo kusaidia kufanikisha malengo yao kwa uharaka zaidi,” alisema Nsekela.


Nsekela alisema katika kuhakikisha wanawake wanapata elimu na usaidizi wa kutosha katika huduma ya CRDB Malkia, Benki ya CRDB imeweka wataalamu wa uwezeshaji wanawake wajulikanao kama “Malkia Rafiki” katika mtandao wa matawi yake yote nchi nzima.


Akihitimisha kongamano hilo, Nsekela alisema kuwa kupitia kauli mbiu ya “Fanikisha Zaidi na CRDB Malkia”, Benki ya CRDB imejipanga vilivyo kushiriki katika safari ya mafanikio ya wanawake wote wa Tanzania na kuwaomba wanawake wajitokeze kwa wingi katika matawi ya Benki ya CRDB ili kuanza kufurahia huduma hiyo mpya ya CRDB Malkia. “Ukifika tawini ulizia Malkia Rafiki naye atakusaidia kuanza safari yako ya mafanikio,” alihitimisha Nsekela.

Kwa mwaka huu hii ni mara ya pili kwa Benki ya CRDB kufanya maboresho katika huduma zake hususani upande wa mikopo, ambapo mwanzoni mwa mwezi Juni, Benki ilizindua kampeni ya mikopo ya wafanyakazi iitwayo “Jiachie Utakavyo” ambapo mteja anapewa uhuru wa kuchagua riba atakayo na muda wa kulipa atakao. Maboresho haya yanakuja wakati muafaka ikiwa wafanyabiashara wengi wakipambana kurudi katika hali ya kawaida baada ya kuathirika na janga la COVID-19.


Send this to a friend