Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amewataka wabunge kutombebesha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mzigo ambao hastahili kwamba hakuahidi kutoa TZS milioni 50 kila kijiji.
Dkt. Tulia amesema hayo bungeni mjini Dodoma na kueleza kuwa katika kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2015, Rais Samia, ambaye wakati huo alikuwa mgombea mwenza hakutoa ahadi hiyo.
“Waheshimiwa wabunge tusianze kumtwika Rais wetu mambo ambayo hajaahidi ikiwa ni pamoja na hili la milioni 50,” amesema kiongozi huyo.
Aidha, Dkt. Tulia amesisitiza kuwa ahadi hiyo haipo hata katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 ambayo ndiyo inatekelezwa sasa baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kushinda.
“Hiyo ahadi haipo, alipita kwenye majimbo yetu na hakusema hivyo,” ameongeza Dkt. Tulia.
Ahadi ya kutoa TZS milioni 50 kila kijiji ilitolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 ambapo aliyekuwa mgombea wa CCM, Hayati Dkt. John Magufuli aliahidi kutoa fedha hizo ili kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.