Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema itasitisha safari za ndege za RwandAir baada ya mamlaka kuishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23.
Kinshasa wiki hii imesema Kigali inaunga mkono Vuguvugu la Machi 23, ambalo Rwanda inakanusha, huku kukiwa na mapigano mapya kati ya jeshi la DR Congo na wanamgambo Mashariki mwa nchi hiyo.
Aidha, Serikali ya DRC inadai kuwa Serikali ya Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23, ikitolea mfano vifaa vya kijeshi vilivyopatikana pamoja na shuhuda kutoka kwa wenyeji na picha zilizonaswa na wanajeshi.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa umesema mapigano ya hivi majuzi kati ya wanajeshi na waasi wa M23 Mashariki mwa DRC yamewakosesha makazi watu 72,000.
Kundi la Watutsi, M23 ni mojawapo ya zaidi ya makundi 120 yenye silaha yanayozunguka Mashariki mwa DR Congo, ambayo mengi ni urithi wa vita vya kikanda zaidi ya miongo miwili iliyopita.