DRC yaifungulia kesi Rwanda Mahakama ya Haki za Binadamu, kesi kusikilizwa leo

0
3

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefungua kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao yake Jijini Arusha ikidai kuwa Rwanda imehusika katika mauaji na uporaji Mashariki mwa DRC kupitia kundi la waasi la M23. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Februari 12, 2025.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa mwaka 2023, Congo inadai kuwa mzozo huo ulioanza mwaka 2021, umesababisha mauaji, uvamizi wa maeneo yake, na watu 520,000 kulazimika kuyahama makazi yao, kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu na uharibifu wa shule na hivyo kusababisha watoto 20,000 kukosa elimu.

Aidha, DRC inalalamikia uharibifu wa miundombinu yake kama vile vifaa vya kusambaza umeme, uporaji na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na vituo vya afya.

Pia inadai kuwa Rwanda inawahifadhi watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa, na ambao mahakama zake zimetoa hati za kimataifa za kukamatwa kwao.

Hayo yanajiri siku chache baada ya Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, na Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC, kukutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo.

Send this to a friend