
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeondoa hitajio la Visa kwa raia wa Tanzania wanaoingia nchini humo kuanzia Machi 20, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani imesema baada ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwezi Julai, 2022, tarehe 2, Septemba 2023 Serikali ya Tanzania iliondoa utaratibu wa malipo ya visa kwa raia wa DRC kwa matarajio ya nchi ya DRC kufuta utaratibu wa kutoza malipo ya visa kwa msingi wa kuungana mkono.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaamini kuwa kwa uamuzi huu wa Serikali ya DRC ni hatua nzuri katika kuimarisha mtangamano na utakuwa na manufaa, ikizingatiwa kuna muingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili katika masuala mbalimbali ya kijamii na kibiashara,” imesema Wizara.
Imeongeza kuwa, “Vilevile kuondolewa kwa hitajio la visa kutachochea ukuaji wa uwekezaji, biashara na kupunguza gharama. ”
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa hatua hiyo ni moja ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na ujirani mwema kwa vitendo.