Elon Musk apendekeza watumiaji wa X kulipia kila mwezi
Mmiliki wa mtandao wa X ambao awali ulikuwa unajulikana kama Twitter, Elon Musk amependekeza kuwa watumiaji wa mtandao huo wanaweza kulazimika kulipa ili kufidia huduma za mtandao huo.
Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, bilionea huyo alisema kuwa mfumo wa malipo ndio njia pekee ya kupambana na matumizi ya akaunti zinazoendeshwa na roboti.
“Tunaelekea kuwa na malipo madogo ya kila mwezi kwa matumizi ya mfumo huu,” amesema Musk ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla na SpaceX.
Mpaka sasa haijulikani ikiwa kauli hiyo ilikuwa ni maoni ya kawaida ya Elon Musk au ni ishara ya mipango thabiti ambayo haijatangazwa rasmi na mtandao huo.
Tangu achukue umiliki wa Twitter mwaka jana Musk ameendelea kuhamasisha watumiaji kulipia huduma iliyoboreshwa, ambayo sasa inaitwa X Premium. Hili limefanywa kwa kuwapa watumiaji wanaolipia vipengele zaidi, kama vile machapisho marefu na kuongezeka kwa mwonekano kwenye jukwaa.