“Energy Drinks zinavyosababisha matatizo ya moyo”. – JKCI

0
60

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imesema katika utafiti wake mpya umebaini unywaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini maarufu ‘energy drinks’ unaweza kuleta madhara kwenye mishipa ya moyo kuziba na hata kusababisha vifo vya ghafla.

Mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Pedro Palangyo amesema utafiti huo unamhusisha kijana wa Kitanzania ambaye mshipa wake mkubwa wa moyo uliziba ghafla kwa asilimia 100, na vijana wengine wakipokelewa ambao wamekuwa wakipata changamoto mfanano na hiyo wakiwa na historia ya kutumia vinywaji hivyo.

“Unapokunywa kinywaji hiki huchukua muda wa dakika kumi hivi caffeine kuingia kwenye mzunguko wa damu, na matokeo yake mapigo ya moyo na shinikizo la damu huongezeka, hivyo kumwondolea mtu uchovu. Lakini ukizidisha hiki kinywaji inaleta athari kwenye mishipa,” ameeleza.

Poda ya watoto ya J&J yadaiwa kusababisha saratani

Aidha, Dkt. Palangyo amesema kijana huyo hakuwa na visababishi vyote vitano hatarishi ambayo ni mgonjwa ya kuambukiza, hakuwa mtumiaji wa sigara na pombe, hakuwa na uzito mkubwa, ulaji wake ulikuwa wa kawaida na mwenye kuzingatia mazoezi. Kitu pekee kilichobainika ni mtumiaji wa ‘energy drinks’ ambapo alikuwa kitumia makopo mawili hadi matano kwa siku.

“Na siku husika alikuwa ametoka kunywa makopo matano ndani ya saa nne. Baada ya kumaliza lile kopo la tano ndipo alipoanza kupata kichomi kwenye moyo, kiliendelea kuwa kikali pamoja na kwamba alimeza dawa za maumivu hakikutulia mpaka alipoletwa kwetu,” ameeleza Dkt. Palangyo.

Hata hivyo Dkt. Palangyo amesema mgonjwa huyo ataendelea kutumia dawa mbalimbali katika maisha yake yote kwa kuwa aliwekewa kifaa kiitwacho ‘stant’ wakati wa kuzibua mshipa huo ili kuhakikisha hauzibi tena.

Taasisi hiyo imeonya kuwa mtu asinywe zaidi ya kopo moja lenye ujazo wa milimita 250 ndani ya saa 24, huku wanywaji wakishauriwa endapo kuna uwezekano wa kuepuka kinywaji hicho wachukue hatua hiyo ili kulinda afya zao.

Send this to a friend