Eng. Hersi akanusha kuwakashifu Yanga kuhusu ulaji mihogo

0
56

Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kupuuza kauli inayosambaa mitandaoni inayotumika kuwakejeli baadhi ya mashabiki wa Yanga wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa matawi jijjni Mwanza.

Kauli hiyo ambayo ilihusisha ‘ulaji wa mihogo’ huku akilenga wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kulalamika juu ya matokeo, amesema lengo halikuwa kuwakejeli mashabiki wa Yanga bali ililenga kuwa na mapenzi na klabu na si matokeo ya klabu.

“Wote waliosikiliza kauli yangu wanaelewa nilikuwa namaanisha nini, ni kauli ambayo ilikuwa inajenga mapenzi na klabu na si mapenzi na matokeo ya klabu, kauli ilikuwa inajenga umoja wa watu kushirikiana kufanya kazi na si vinginevyo, naomba kauli hiyo ipuuzwe na sisi kama Young Africans tusimame katika njia ya kuijenga timu yetu na kujenga mshikamano wetu,” amesema.

Aidha, Hersi amesema baada ya mchezo dhidi ya Club Africain kumalizika Novemba 2, 2022 jijini Dar es Salaam na kutoka suluhu, viongozi wa klabu hiyo wamepokea maoni ya wanachama, mashabiki na wapenzi na kuahidi kuyafanyia kazi.

Hata hivyo, amewataka wanachama na wapenzi wa Yanga kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wao, benchi la ufundi na viongozi ili kuhakikisha wanakwenda kufanya yale ambayo wananchi wanayatarajia katika mchezo wa marudiano dhidi ya Club Africain Novemba 9 mwaka huu nchini Tunisia.

Send this to a friend