Eng. Hersi: Feisal bado hajarudi kambini, anadanganywa

0
43

Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said amesema mpaka sasa mchezaji wa klabu hiyo Feisal Salum hajaripoti kambini kuendelea na majukumu yake hivyo kama klabu bado inaendelea kumkumbusha kuwa anatakiwa kurudi kambini hapo.

Akizungumza katika mahojiano katika kipindi cha Clouds 360, Eng. Hersi amesema matakwa ya kimkataba yanamhitaji mchezaji huyo ili kulipa stahiki zake katika kipindi chote ambacho hakuwepo.

“Sisi Feisal ni mchezaji wetu, ni kijana wetu. Suala hili linaloendelea kuna watu wanaweza kuwa wanaongeza chumvi nyingi huko kwenye mitandao, sisi kwetu hicho kitu siyo muhimu tuna mkataba na mchezaji mpaka 2024,” ameeleza.

Aidha, amesema kama kuna mtu ambaye anamlaghai mchezaji huyo anapaswa kupigwa vita kwa kuwa kuna utaratibu wa kufuata ikiwa mchezaji atahitajika na si kupita nyuma ya pazia.

Hata hivyo ameeleza kuwa endapo mchezaji huyo ataamua kurudi kambini, atapokelewa kwa mikono miwili na kupewa sapoti yote ili kutimiza majukumu yake kama mchezaji.

Send this to a friend