Epuka kula vyakula hivi wakati wa kufuturu/kufungua

0
14

Katika kipindi hiki ambapo Waislamu na Wakristo wako katika mfungo wa Ramadhan na Kwaresma, vyakula mbalimbali huandaliwa ili kutumika kwa ajili ya kufuturu/kufungua.

Hata hivyo, wataalam wa afya wamewataka wananchi kuwa makini na aina ya vyakula wanavyotumia wakati wa kufuturu/kufungua, wakisisitiza kuwa ulaji usiofaa unaweza kusababisha matatizo ya mmeng’enyo wa chakula na kuathiri afya kwa ujumla.

Hivi ni aina ya vyakula ambavyo havishauriwi kutumika wakati wa kufuturu/kufungua kwa mujibu wa wataalamu wa afya;

Vyakula vya mafuta mengi na vya kukaanga
Vyakula kama chipsi, samosa, maandazi ya kukaanga na nyama zilizojaa mafuta huweka mzigo mkubwa kwenye tumbo ambalo limekuwa tupu kwa muda mrefu. Ulaji wa vyakula hivi wakati wa kufuturu/kufungua kunaweza kusababisha kiungulia, gesi tumboni, maumivu ya tumbo na kuongezeka kwa uzito.

Vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi
Soda, juisi zenye sukari nyingi, keki na pipi husababisha kiwango cha sukari kupanda haraka mwilini na baadaye kushuka ghafla. Hali hii inaweza kuleta uchovu, kizunguzungu na njaa ya haraka muda mfupi baada ya kufuturu.

Vyakula vyenye chumvi nyingi
Vyakula vya makopo, nyama zilizosindikwa na vitafunwa vyenye chumvi nyingi huongeza kiu na vinaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini, hasa kama mtu hakunywa maji ya kutosha. Pia chumvi nyingi huongeza shinikizo la damu mwilini.

Ulaji wa chakula kingi kwa wakati mmoja
Kula chakula kingi baada ya kufunga huathiri mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na kusababisha tumbo kujaa kupita kiasi, uvimbe na maumivu. Wataalam wanashauri kula kwa hatua na kwa kiasi.

Vinywaji vyenye kafeini nyingi
Unywaji wa kahawa au chai nyingi mara tu baada ya kufuturu unaweza kuongeza upotevu wa maji mwilini na kuathiri usingizi, hasa endapo vitatumika kwa wingi.

Send this to a friend