Esther Matiko: Rais Samia ameendeleza miradi ya kimkakati kwa ufanisi mkubwa

0
15

Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko amesema Rais Samia Suluhu ameweza kuendeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya kimkakati aliyoiacha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli licha ya kupitia changamoto ya kuyumba kwa uchumi wa kidunia.

Ametoa pongezi hizo leo Juni 22, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Sote tunajua mazingira yaliyotokea Tanzania ambapo tulipotelewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Rais Magufuli, na akawa ameacha miradi mingi ya kimkakati ambapo wengi wetu walibeza, labda nafikiri kwa sababu ya ujinsia wake, lakini mama ameweza kuendeleza miradi hii kwa ufanisi mkubwa sana pamoja na kwamba kuna kuyumba kwa uchumi duniani lakini mama ameweza kufanikisha na mambo yote yanaenda,” amesema.

Aidha, Matiko amempongeza Rais kwa kuimaeisha demokrasia na uhuru wa kujieleza kwa kuruhusu mikutano ya hadhara, pia akitolea mfano wa Siku ya Wanawake Duniani ambayo alisherehekea na Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) ikiwa ni mara ya kwanza kwa jambo hilo kufanyika nchini.

“Kwakweli hii inajenga confidence [kujiamini] sio tu kwa vyama vya upinzani bali hata kwa wawekezaji, na hata mataifa mengine tumeona uhusiano umekuwa chanya sana, hii pia inaweza kujenga confidence na watu kuja kuendelea kuwekeza  Tanzania na kuweza kuona maendeleo yanatamalaki,” ameeleza Matiko.

Send this to a friend