EWURA: Bei ya mafuta itaendelea kupanda

0
36

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imesema kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa mafuta, bei ya mafuta inatarajiwa kuendelea kupanda zaidi hali inayochangiwa na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, huku usafirishaji na upokeaji wake nchini kuwa hafifu.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Godfrey Chibulunje alipokuwa katika mdahalo uliohusisha Wahariri na waandishi wa habari hapo jana alisema kuwa, mfumuko wa bei unasababishwa na changamoto mbalimbali inayoikumbuka miundombinu ya usafirishaji kutoka na sababu za kivita.

Alibainisha kuwa katika soko la dunia bei ya mafuta imepanda kwa kiasi kikubwa, huku akieleza kuwa mwezi Desemba 2021 tani moja ya mafuta ya petroli ilikuwa inauzwa dola 717, na hadi kufikia Machi mwaka huu ilipanda hadi kufikia dola 1,106 kwa tani moja.

“Bei za mafuta zinatofautiana sana katika maeneo mbalimbali duniani, barani Afrika, Ulaya na Amerika, wakati Tanzania lita moja ya dizeli ikiwa inauzwa TZS 2,403, Kenya ni 2,331 na Uganda 2,830, hivyo ukiangalia nchini kulikuwa na unafuu kwa kiasi fulani,” amesema

Aidha aliongeza kuwa kesho watatangaza bei mpya ya mafuta na mara baada ya vita kuisha hali itarudi kuwa shwari.

Pia aliwataka Watanzania kujiwekea utaratibu mzuri katika matumizi ya mafuta na kuangalia njia mbadala kama kuanza kufikifria kutumia magari yanayotumia gesi na umeme ili kuendesha shughuli zao.

Alisema kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya upokeaji wa mafuta bandarini ili kutatua changamoto zilizoko ndani ya uwezo wake na EWURA itaendelea kusimamia mwenendo wa uuzwaji wa mafuta hayo.

Send this to a friend