EWURA kuzifutia leseni kampuni tano za mafuta

0
22

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kusudio la kuzifutia leseni kampuni tano za utoaji huduma za mafuta kutokana na tuhuma kuwa zimehusika kutengeneza uhaba wa bidhaa hizo nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Tito Kaguo amesema kuwa kampuni hizo zimeficha mafuta wakati huu ambapo bei imeshuka hivyo kupelekea upungufu wa mafuta na kusababisha taharuki isiyo na lazima kwa watumiaji wa bidhaa hizo.

Watoa huduma waliopo hatarini kupoteza leseni zao ni Moil, Olympic Petroleum Tanzania Limited, B.O Five Ways Petroleum Stations ya Bagamoyo, Mexon Energy Limited ya Makambako na Mexon Energy ya Njombe.

“Haitochukua muda kabla hatujafuta leseni za watoa huduma hawa. Tunatangaza kusudio kwa sababu sheria, kanuni na taratibu za EWURA zinatutaka kufanya hivyo,” amesema Kaguo.

Hatua ya kufuta leseni za watoa huduma hao imetokana na mamlaka hiyo kutoridhishwa na maelezo waliyotoa juu ya kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kutengeneza upungufu wa mafuta, ambapo jumla ya kampuni 10 zilitakiwa kuwasilisha maelezo ndani ya saa 48 kuanzia Juni 22 mwaka huu.

Bei ya mafuta imeshuka kwa kiasi kikubwa katika miezi michache iliyopita ambapo kwa mujibu wa EWURA hali hiyo imechangiwa na kupungua kwa uhitaji kulikosababishwa na mlipuko wa janga la virusi vya corona lililopelekea kusitishwa kwa shughuli nyingi za usafiri na usafirishaji.

Kwa wakazi wa Dar es Salaam sasa wanalipa TZS 1,520 kwa lita moja ya petroli na TZS 1,546 kwa lita ya dizeli, bei ambazo ni ndogo zaidi kuwahi kuwepo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.