Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeutaarifu umma kuwa nchi ina mafuta ya kutosha katika maghala ya kuhifadhia mafuta.
Vile vile imesema meli zenye shehena ya mafuta kutoka nje ya nchi zinaendelea kuingia na kushusha mafuta kama kawaida chini ya uratibu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Tamko hilo ni kufuatia taarifa ya uwepo wa baadhi ya kampuni za mafuta kuhodhi mafuta kwa ajili ya maslahi binafsi ya kibiashara ikiwemo kusubiri mabadiliko ya bei, pia taarifa madai ya kampuni nyingine kupakia mafuta kutoka kwenye maghala pasipo kuyauza na kukataa kuuza mafuta kwa wamiliki wa vituo wasiokuwa na ubia nao.
EWURA imesema mpaka Julai 14 mwaka huu, mafuta yote yaliyokuwepo nchini ni lita 169,853,692 za mafuta ya petroli, lita 209,641,670 za dizeli na lita 34,588,002 za mafuta ya ndege yanayotosheleza mahitaji.
“Kutokana na taarifa hizo, EWURA inatoa onyo kwa kampuni za mafuta zinazohodhi mafuta na kuzitaka kuacha mara moja, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta ya petroli nchini na masharti ya leseni zao za biashara,” imesema taarifa ya EWURA.
Aidha, imesema inaendelea kufanya ukaguzi wa kina kwenye maghala na vituo vya mafuta, na hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaothibitika ikiwemo kuwanyang’anya leseni za biashara.