EWURA yavifungia vituo vya mafuta kwa kuficha mafuta

0
44

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imevifungia vituo vya mafuta vya Camel Oil (Msamvu) na kituo cha Matemba (Turiani) vilivyopo mkoani Morogoro, kutojishughulisha na uuzaji mafuta kwa kipindi cha miezi sita kutokana na kuhodhi mafuta kinyume cha sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile amesema vituo vingine 16 vinafanyiwa uchambuzi kwa mujibu wa sheria na endapo EWURA itajiridhisha kwamba vimekiuka sheria na masharti ya leseni, vituo hivyo vitachukuliwa hatua kali ikiwemo kufungiwa.

“Nitoe onyo kwamba, kiwe ni kituo cha mafuta, iwe ni wenye maghala ambao tumewapa leseni, iwe ni waagizaji wa mafuta ambao tumewapa leseni, ikithibitika kwamba umeshikilia mafuta kinyume na taratibu, kwa mamalaka ambayo EWURA imepewa kisheria itakuchukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Ameongeza, “baada ya hii adhabu ambayo EWURA imetoa, haitaishia hapa, kwa sababu suala la kuhodhi mafuta ni mwelekeo wa kuhujumu uchumi wa nchi na tutawasilisha taarifa hizo kwa DCI, na kwa mwendesha mashtaka wa serikali ili wakjiridhisha wawachukulie sheria ya uhujumu uchumi,” amesema.

ACT-Wazalendo yaunga mkono uwekezaji wa DP World yatoa mapendekezo

Aidha, EWURA imethibitisha kuwa kuna mafuta ya kutosha kwenye maghala pamoja na ambayo yako kwenye meli zilizowasili bandarini zikisubiri nafasi ya kuingia kwenye gati na kushusha mafuta hayo.

“Kwa mafuta yaliyopo kwenye maghala na yale yaliyopo kwenye meli zilizowasili, nchi ina mafuta yatakayokidhi mahitaji ya siku 19. Pamoja na mafuta hayo, meli zitaendelea kuwasili hadi tarehe 31 Oktoba 2023 kulingana na mpangilio ulioainishwa katika zabuni za uagizaji wa mafuta kwa pamoja (BPS) zilizofanyikakufikia tarehe 31 Agosti 2023,” amesema.

Send this to a friend