Kwikwi hutokana na kushtuka na kusinyaa ghafla kwa misuli mikuu ya upumuaji (diaphragm) ambako hujirudia rudia na kusababisha hewa kuingia kwa kasi kwenye mapafu.
Hii husababisha milango ya sauti katika koo kufunga ghafla na kutoa sauti inayosikika wakati wa kwikwi.
Kwikwi sio ugonjwa, kwikwi ya muda mfupi ni kero ndogo tu ambayo inapita, lakini kwikwi isiyokatika kwa muda mrefu inaweza kuwa dalili ya tatizo jingine ambalo huenda likahitaji uchunguzi wa kitaalamu.
Mara chache kwikwi za muda mrefu ambazo zinadumu kwa mwezi mmoja au zaidi zinaweza kutokea na kama kwikwi ikiendelea kwa zaidi ya saa 48 basi unahitaji msaada wa daktari kwani hii inaweza kuwa ni ishara ya tatizo kubwa la kiafaya.
Sababu zinazopelekea kupata kwikwi ni pamoja na kula haraka haraka au kula sana (kuvimbiwa), kula vyakula vyenye viungo sana, kunywa vinywaji vyenye gesi au vya baridi sana, ulevi au kunywa pombe nyingi kwa mpigo, upungufu wa maji na madini mwilini na tumbo kujaa gesi, asidi au vidonda vya tumbo.
Namna ya kuzuia kwikwi;
Kula taratibu: Kula haraka haraka husababisha kujaa kwa gesi tumboni na kusababisha kuvimbiwa.
Kula kiasi kidogo kwa wakati: Inashauriwa kuongeza idadi ya milo kwa siku badala ya wingi wa chakula. Kula milo mitano midogo midogo badala ya mitatu mikubwa kwa siku.
Punguza au ondoa kabisa vyakula vyenye viungo vingi au vikali.
Unywaji wa maji utakusaidia kuzuia na kutibu kwikwi.
Fanya mazoezi. Hii itaboresha ufanyaji kazi wa mapafu na misuli ya upumuaji
Namna nyingine ya asili inayotumiwa kuondokana na kwikwi unapokuwa nyumbani ni pamoja na kunywa glasi ya maji iliyojaa bila kukata pumzi, kubana pumzi na kuhesabu mpaka kumi, kuweka sukari chini ya ulimi na kulala singizi.