Fahamu chanzo cha mgogoro kati ya Iran na Israel

0
107

Mgogoro kati ya Iran na Israel ni sehemu ya mizozo ya muda mrefu katika eneo la Mashariki ya Kati. Mizizi ya mgogoro huu inahusisha mambo ya kihistoria, kidini, kisiasa, na kijiografia.

Uhusiano kati ya Israel na Iran ulikuwa wa kuridhisha hadi ilipofika mwaka 1979 baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Ayatollahs huko Tehran. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalibadilisha utawala wa Iran kutoka utawala wa kifalme uliyoongozwa na Shah Reza Pahlavi na mmoja wa washirika wakuu wa Marekani kwenda serikali ya Kiislamu inayoongozwa na Ayatollah Ruhollah Khomeini.

Baada ya mapinduzi hayo, Iran ilianza kufuata sera za Kislamu zenye msimamo mkali na kuanza kutoa msaada kwa makundi ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati. Uhusiano baina ya Iran na Israel haukuwa na uadui kwani Iran ilikuwa moja ya nchi za kwanza za Kiislamu kulitambua taifa jipya la Israel baada ya kugawanywa kwa Palestina mwaka 1948.

Hata hivyo, utawala mpya wa Ayatollah ulivunja uhusiano na Israel, ukaacha kutambua uhalali wa hati za kusafiria za raia wa Israel na ukauteka ubalozi wa Israel mjini Tehran ili kuukabidhi kwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) ambayo wakati huo ilikuwa ikiongoza mapambano ya kulipigania taifa la Palestina dhidi ya serikali ya Israel pamoja na kutoa msaada wa kifedha na kijeshi kwa makundi ya Kipalestina.

Ayatollah alilibeba suala la Palestina kama lake mwenyewe na maandamano makubwa ya kuunga mkono Wapalestina yakawa yanafanyika mara kwa mara mjini Tehran.

Baada ya muda, Israel ilianza kuiona Iran kama hatari zaidi kwa kuwepo wake, hatimaye uhasama kati ya nchi hizo ulitoka kuwa wa maneno hadi kuwa wa vitendo ambapo Israel ilifanya mashambulizi na operesheni dhidi ya Iran na washirika wake mara nyingi katika nchi ambako Iran inafadhili na kuunga mkono makundi yenye silaha.

Mpaka sasa, Israel inaishutumu Iran kwa kufadhili vikundi vya kigaidi na kufanya mashambulizi dhidi ya maslahi yake, huku vita vya Gaza vikifanya mambo kuharibika zaidi.

Send this to a friend