Fahamu haki za mtuhumiwa anapokamatwa na polisi

0
31

Mara nyingi watu wamekuwa wakikamatwa, na katika matukio hayo huenda wakamataji wakakiuka haki za anayekamatwa ambaye pia huenda asijue kwa sababu hajui haki zenyewe ni zipi.

Mtuhumiwa, (mtu yeyote ambaye anawekwa chini ya ulinzi na polisi au chombo cha usalama kwa kutuhumiwa kufanya kosa) ana haki za msingi ambazo ni lazima zizingatiwe wakati wa kukamatwa ambazo ni pamoja na:

(a) Mtuhumiwa anapowekwa chini ya ulinzi ana haki ya kuelezwa sababu za kukamatwa au kutiliwa mashaka.

(b) Mtuhumiwa ana haki ya kudai risiti ya orodha ya vyombo/mali atakayokuwa nayo wakati wa kumpekua zile zinazochukuliwa kituoni na pale anapokabidhiwa polisi.

(c) Mtuhumiwa akiwa mwanamke lazima kukaguliwa na polisi mwanamke.

(d) Mtuhumiwa ana haki ya kudai kibali cha hakimu pale majadiliano/maelezo kwa polisi yanapozidi saa nane.

(e) Mtuhumiwa anayo haki ya kudai awasiliane na mtu anayemtaka akiwa chini ya ulinzi. Kwa mfano rafiki, ndugu au wakili.

(f) Mtuhumiwa ana haki ya kufikishwa mahakamani katika muda usiozidi masaa 24

(g) Mtuhumiwa ana haki ya kukaa kimya wakati wa mahojiano na polisi na anapaswa kuelezwa kwamba chochote ambacho mtuhumiwa atawaeleza polisi inaweza kutolewa mahakamani kama ushahidi dhidi yake.

(h) Mtuhumiwa ana haki ya kutojibu maswali ya polisi na kukaa kimya hadi polisi anayemuuliza/endesha mahojiano awe amemueleza mtuhumiwa yafuatayo:

(i) cheo alicho nacho na jina lake
(ii) mtahadharishwa kwamba yuko chini ya ulinzi.
(iii) kosa alilofanya au sababu ya kuwa chini ya ulinzi.
(iv) anayo haki ya kudai asomewe kilichoandikwa kabla ya kuweka sahihi kwenye maelezo.

(i) Mtuhumiwa anayo haki ya kupewa heshima na kuthaminiwa kwamba ni binadamu. Hakuna ruhusa kumtesa mtuhumiwa na kumdhalilisha anayo haki ya kudai matibabu.

(j) Mtuhumiwa anaweza akaomba dhamana wakati yuko chini ya ulinzi wa polisi.

Chanzo: Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania