Fahamu kazi ya Tufaa la Adam inayoonekana zaidi kwa wanaume

0
67

Tufaa la Adam (Adam’s Apple), nundu inayoonekana shingoni hasa kwa wanaume, ambayo kitaalamu ni prominentia laryngea, kazi yake kuu ni kulinda kisanduku cha sauti (larynx) ili isiharibiwe na majeraha na shinikizo.

Nundu hii huwa kubwa zaidi kwa wanaume kutokana na ongezeko la homoni ya testosterone wakati wa kubalehe, ambayo husababisha kuongezeka kwa sanduku la sauti (larynx) na kuleta mabadiliko kwenye sauti kuwa nzito zaidi.

Kwanini imeitwa Tufaa la Adam?
Jina Tufaa la Adam ‘Adam’s apple’ linatokana na hadithi ya kidini kutoka kwenye maandiko ya Kikristo, Kiyahudi, na Kiislamu. Hadithi hiyo inasema kwamba Adamu, mtu wa kwanza, alikula tunda lililokatazwa kwenye Bustani ya Edeni.

Ingawa tunda halikuelezwa moja kwa moja kama tufaa (apple), tamaduni nyingi zimehusisha tunda hilo na tufaa. Inadaiwa kipande cha tunda kilikwama kwenye koo la Adam, na hivyo nundu hiyo kwenye shingo za wanaume ikaitwa Tufaa la Adam. Hata hivyo hakuna uthibitisho wowote wa kisayansi juu ya hadithi hiyo.

Je, kutoonekana kwa tufaa la Adam kunaweza kuleta athari?
Kwa kawaida, kuwa na Adam’s apple ndogo au isiyoonekana haina madhara makubwa kiafya. Mwanaume ambaye haionekani sana bado anaweza kuwa na kamba za sauti zinazofanya kazi vizuri. Ukubwa wa nundu hii hutofautiana kati ya watu, na haina uhusiano wa moja na matatizo ya sauti.

Wanawake pia wanaweza kuwa na nundu kama wanaume?
Wanawake pia wanaweza kuwa na nundu hii ingawa kwa kawaida ni ndogo na haionekani kama ilivyo kwa wanaume. Hii inatokana na tofauti za homoni na ukuaji wa larynx wakati wa kubalehe.

Wakati wa kubalehe, homoni za kiume (hasa testosterone) huchangia kuongezeka kwa ukubwa wa larynx kwa wanaume, na hivyo kufanya Adam’s apple kuonekana zaidi. Wanawake, ingawa pia wanapata mabadiliko ya sauti wakati wa kubalehe, larynx yao haina ongezeko kubwa kama la wanaume, hivyo nundu hiyo mara nyingi ni ndogo au haionekani sana.

Inaweza kuondolewa au kupunguzwa?
Kuna utaratibu wa upasuaji wa kupunguza ukubwa unaoitwa chondrolaryngoplasty au tracheal shave. Hii ni aina ya upasuaji wa urembo kwa watu ambao wanahisi nundu hiyo inajitokeza sana.

Upasuaji huu ni salama kwa ujumla, lakini kama ilivyo kwa upasuaji wowote, kuna hatari kama vile kuathiri sauti au kusababisha maambukizi.

Send this to a friend