Fahamu kuhusu shambulio la hofu (Panic attack) linalowakumba watu wengi bila kujua

0
61

Shambulio la hofu (Panic attack) ni hali ya ghafla na ya woga au wasiwasi ambayo mtu anaweza kupata bila sababu yoyote ya wazi. Hali hii inaweza kudumu kati ya dakika tano hadi ishirini, lakini wakati mwingine inaweza kudumu zaidi.

Shambulio la hofu hutokea mara kwa mara na wakati mwingine ukiwa umelala pasipo kutarajia na mara nyingi hayahusiani na tishio lolote la nje.

Dalili za shambulio la hofu ni pamoja na;

1. Mapigo ya moyo kuwa ya kasi au kupiga kwa nguvu.
2. Kupumua kwa shida au kwa haraka (hyperventilation).
3. Kujihisi joto kali au baridi.
4. Kujihisi kizunguzungu au kama utaanguka.
5. Kutetemeka.
6. Hofu ya kupoteza udhibiti, kufa, au kuhisi kama uko kwenye hali isiyo halisi (derealization).

Mara nyingi, ‘panic attacks’ hutokea ghafla, na huwa na nguvu kiasi kwamba mtu anaweza kuhisi kama anakabiliwa na hatari ya kifo. Sababu za tatizo hili hazieleweki kabisa, lakini zinaweza kuchangiwa na msongo wa mawazo (stress), historia ya familia ya magonjwa ya akili, au kutokea kwa matukio ya kushtukiza katika maisha ya mtu.

‘Panic attacks’ zinaweza kutokea kama sehemu ya matatizo ya wasiwasi yanayoitwa panic disorder, lakini pia zinaweza kutokea hata bila kuwa na tatizo hilo.

Matibabu ya ‘panic attack’ yanaweza kujumuisha tiba ya kisaikolojia, kama vile tiba ya kitabia (Cognitive Behavioral Therapy – CBT), na matumizi ya dawa kama vile zile za kupunguza wasiwasi.

Pia, kuna mbinu mbalimbali za kujisaidia kupunguza athari ya panic attack, kama vile kujifunza kupumua kwa utulivu, kufanya mazoezi ya kupunguza msongo wa mawazo, na kubadilisha mtazamo wa mambo yanayosababisha woga.

Ni muhimu kumuona daktari kwa uchunguzi ili kuhakikisha kuwa dalili zozote za kimwili zinazojirudia na kufanana na panic attack hazisababishwi na magonjwa mengine, ikiwemo kisukari, pumu (asthma), shida za ndani ya sikio, Hyperthyroidism (tezi la thyroid kufanya kazi kupita kiasi) na shida za moyo.

Send this to a friend