Fahamu maana ya madaraja ya leseni ya udereva
Leseni ya udereva ni hati ya kisheria inayomruhusu dereva kuendesha chombo katika daraja lililooneshwa katika leseni hiyo.
Leseni hubeba taarifa mbalimbali zinazomhusu dereva kama vile picha, namba ya leseni, majina matatu ya mwenye leseni, tarehe inayoonyesha leseni imetolewa lini na muda wake wa kuisha.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mfumo wa leseni za udereva una makundi mbalimbali kama ifuatavyo;
•Vyombo binafsi vya moto
B- Leseni ya kuendesha aina zote za vyombo vya moto isipokuwa pikipiki, magari ya biashara, magari makubwa na magari ya kutoa huduma kwa jamii.
•Magari ya kutoa huduma kwa umma
C- Leseni ya kuendesha magari ya kutoa huduma kwa jamii yenye uwezo wa kubeba abiria 30 na zaidi pamoja na dereva. Magari katika kundi hili yanaweza kufungwa tela lenye ujazo wa juu unaokubalika usiozidi kilo 750.
Hata hivyo waombaji wanatakiwa wawe wamewahi kuwa na leseni ya daraja la C1 au E kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
C1 ni leseni ya kutoa huduma kwa umma yenye uwezo wa kubeba abiria 15 na wasiozidi 30, abiria pamoja na dereva. Waombaji wanatakiwa wawe wamewahi kuwa na leseni ya daraja D kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
C3- Leseni za kuendesha magari ya kutoa huduma kwa umma yenye uwezo wa kubeba abiria wanne au pungufu akiwemo dereva. Waombaji wanatakiwa wawe wamewahi kuwa na leseni ya daraja D kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
•Magari madogo ya mizigo ya biashara
D- Leseni ya kuendesha aina zote za vyombo vya moto isipokuwa pikipiki, magari makubwa na magari ya kutoa huduma kwa umma.
•Magari makubwa ya mizigo ya biashara
E- Leseni ya kuendesha aina zote za vyombo vya moto isipokuwa pikipiki na magari ya umma. Waombaji wanatakiwa wawe wamewahi kuwa na leseni ya daraja D kwa muda usiopungua miaka mitatu.
•Magari yenye trela
F- Leseni ya kuendesha magari yanayokokota trela.
•Magari ya shambani na migodini
G- Leseni ya kuendesha magari ya shambani na migodini.
•H- Leseni ya muda ya kujifunza.
Hii ni leseni kwa wale ambao wanajifunza udereva.
Mwombaji yeyote wa leseni ya udereva ni lazima awe na umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na awe amepitia mafunzo ya udereva kwa taasisi inayotambulika.
Chanzo: Mwananchi.